Rais Jakaya Kikwete, amekemea vikali baadhi ya vikundi vya dini vinavyofanya mihadhara ya kukashifu dini nyingine. Rais Kikwete amesema kufanya hivyo ni kupandikiza chuki miongoni mwa jamii.
Rais Kikwete alitoa karipio hilo jana Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa 59 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Alisema serikali itachukua hatua za kisheria ikiwa vikundi hivyo vitaendelea kufanya mahubiri ya namna hiyo dhidi ya dini nyingine.
Alisema badala ya mihadhara hiyo kuwaelimisha wananchi, inageuka kuwa majukwaa ya kukashfia dini za waumini wengine.
’’Hali hii hatuwezi kuiacha iendelee, tunawashauri wanaofanya hivyo waache mara moja tabia hiyo, wakiendelea, tutawachukulia hatua bila kujali wanatoka dini gani,’’ alisisitiza Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa, Serikali haina dini, lakini wananchi wana uhuru wa kuabudu dini yoyote wanayoitaka.
Rais Kikwete alisema hata kama kuna mambo yanayofanywa na dini nyingine hayawafurahishi wengine, wananchi wanapaswa kuwa na moyo wa kuvumiliana.
Kuhusu amani na usalama nchini, Rais Kikwete alisema hivi sasa ni ya kuridhisha baada ya hatua za kubadilisha uongozi ndani ya Jeshi la Polisi.
’’Kwa kweli nafurahishwa na kazi inayofanywa na viongozi wa Jeshi la Polisi kwa sababu mtandao wa ujambazi sasa unafikia mwisho, kilichobaki ni kuvunja uti wa mgongo wa mtandao huo,’’ alisema.
Alisema uongozi mpya wa jeshi hilo umeonyesha uwezo mkubwa wa kukabiliana na mtandao huo jambo ambalo limesababisha watuhumiwa wengi kukamatwa.
’’Kwa hilo nawahakikishieni Maaskofu kwamba, hatuna mchezo, majambazi yamekwi shadhibitiwa, hayatambi tena kwa sababu viongozi wao karibu wote wamekwishakamatwa,’ alisema.
Rais Kikwete aliwaomba viongozi wa dini kwa kushirikiana na serikali kuihamasisha jamii kuwa na maadili mema.
’’Matukio yote ya uvunjaji wa sheria yanayofanywa na jamii yetu, pia yanakatazwa na dini zote, hivyo viongozi wa dini msichoke kuielimisha jamii kuachana na matendo mabaya,’’ alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Severin NiweMugizi, aliipongeza Serikali kwa ushirikiano mkubwa na taasisi za dini hususan katika utoaji wa huduma za jamii.
Aliiomba serikali isaidie katika maslahi kwa wafanyakazi wa vituo vya afya vya Kanisa hilo, kwani wengi wanaondoka kufuata maslahi bora katika hospitali za serikali.
’’Tunayo hofu kwamba hali hiyo ikiendelea itaathiri sana vituo vyetu katika utoaji wa huduma, atakayeumia hatimaye ni mwananchi wa kawaida anayeishi vijijini,’’ alisema.