WANANCHI katika miji kadhaa wamepokea kwa furaha na kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uteuzi mpya wa Baraza la Mawaziri.
Katika Manispaa ya Dodoma, Dunstan Bahai anaripoti kuwa jana kabla ya kutangazwa kwa Baraza la Mawaziri, wananchi walikuwa na shauku kubwa ya kulielewa kwani walikusanyika sehemu zenye radio na televisheni.
Makundi makubwa ya watu yalionekana kwenye migahawa na hata sehemu zenye vinywaji ambako kuna radio na televisheni ambapo mara baada ya kutangazwa, walipokea kwa furaha uteuzi huo.
Wengi walipongeza baadhi ya mawaziri walioteuliwa kwenye baadhi ya wizara na kueleza kuwa wanastahili kabisa na Rais Kikwete hakukosea.
Baadhi ya mawaziri waliopongezwa na wakazi hao ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje itakayoongozwa na Dk. Asha-Rose Migiro, Wizara ya Fedha itakayoongozwa na Zakia Meghji na Wizara ya Mambo ya Ndani chini ya John Chiligati.
Akipongeza uteuzi huo, mkazi wa Chamwino, Ali Jumaa alisema baadhi ya wizara, Rais Kikwete amefanya uteuzi halali kabisa.
Hashimu Sanwia mkazi wa Nkuhungu alipongeza uteuzi wa Waziri wa Afya Profesa David Mwakyusa na kumuelezea kuwa ni mtaalamu wa eneo hilo na kwamba si uteuzi wa kisiasa.
Alisema kuwa matatizo makubwa yanayojitokeza kwenye hospitali kubwa kama Muhimbili yatakuwa yanapata utatuzi kwani waziri huyo ni mzoefu hasa katika hospitali ya Muhimbili ambako alifanya kazi kama mtawala.
Ashura Samson kwa upande wake alipongeza mabadiliko yaliyofanywa kwenye baadhi ya wizara kama Wizara ya Ushirika na Masoko.
Alisema, masoko kuhamishiwa Wizara ya Viwanda ni sahihi na ushirika kuhamishiwa kilimo nalo ni jambo la msingi kabisa kwani vitu hivyo vina uhusiano wa karibu sana.
Kuhusu suala la Muungano, Ashura Hassan alifurahishwa na kuwa na matumaini makubwa kwa kuwa na Waziri anayehsughulikia suala la Mungano ambaye ni Dk. Hussein Mwinyi.
Alisema kumekuwa na matatizo mengi ya Muungano hasa upande wa Zanzibar na kuwepo kwa waziri maalumu wa kushughulikia suala hilo, hali hiyo itaondoa manung'uniko yanayojitokeza.
Kutoka Moshi Rodrick Makundi, anaripoti kuwa muda mfupi baada ya Rais Kikwete kutangaza Baraza la Mawaziri, viongozi wa kisiasa, wanachama na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamepongeza uteuzi huo na kwamba baraza hilo litatekeleza majukumu yake kwa ari, nguvu na kasi mpya.
Katika hatua nyingine, wananchi hao wameonyesha kuridhishwa na uteuzi wa Rais ambao amewateuwa wabunge sita wa Mkoa wa Kilimanjaro kuingia katika baraza hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walidai kuwa serikali ya awamu ya nne, itakuwa na mafanikio makubwa kutokana na viongozi wake kuwa ni wasomi na wenye hoja za msingi ambazo zitatumika katika kuinua maisha ya Watanzania pamoja na kuendeleza mafanikio ya serikali.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Simon Nchimbi alizungumzia uteuzi huo na kusema kuwa inaonyesha nia thabiti ya Chama Cha Mapinduzi katika kuleta maendeleo ndani ya mkoa huo.
"Naomba waelewe kabisa kuwa wakati wa kampeni tuliwaahidi watu kuwa iwapo CCM itaingia madarakani basi mambo mengi yatatendeka na hata vingozi wake watakuwa karibu zaidi na CCM, hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kuwasilisha hoja zao,"alisema.
Aliongeza kuwa hatua ya kuwa na mawaziri watatu pamoja na manaibu waziri watatu ni sawa na mrija wa kupitisha maendeleo katika majimbo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Mpiga debe mkuu wa CCM katika jimbo la Moshi Vijijini na majimbo mengine ndani ya mkoa Thomas Ngawaiya alisema kuwa uteuzi huo ni ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.
"Hiyo ndiyo ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya ambayo CCM inaelezea," alisema Ngawaiya akionyesha kufurahia ushindi muda mfupi kabla ya kukata simu. Alizungumza kwa njia ya simu.
Mkoa wa Kilimanjaro umefanikiwa kuwa na wabunge wa CCM kutoka katika majimbo nane kati ya majimbo tisa ya uchaguzi kwenye uchaguzi uliofanyika Desemba 14, mwaka jana.
Katika wabunge hao wakiwemo wale wa viti maalumu kwa mujibu wa Rais Kikwete, Zakhia Meghji ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba Waziri wa Miundombinu, Profesa Jumanne Maghembe Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana.
Kwa upande wa manaibu waziri mbunge wa viti maalumu Salome Joseph Mbatia ameteuliwa Naibu Waziri wa Mipango na Uchumi, Dk. David Mathayo Naibu Waziri wa Viwanda na Dk. Cyrill Chami ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Mambo ya Nje.
Dk. Chami ni mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini, Dk. Mathayo mbunge wa Same Magharibi, Profesa Jumanne Maghembe mbunge wa Mwanga, wakati Zakhia aliteuliwa na rais kuwa mbunge na Salome mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro.
Awali katika serikali ya awamu ya tatu Waziri Zakhia alikuwa wa Utalii na Maliasili, Salome Joseph Mbatia mbunge Viti Maalum na Profesa Maghembe alikuwa mbunge wa jimbo la Mwanga huku Dk. Chami alikuwa mshauri msaidizi wa rais katika masuala ya uchumi.
Katika hatua nyingine, Furaha Omary, anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa wananchi wamesema wamefurahishwa na uteuzi uliofanywa kwa kuwapa kipaumbele wanawake kama alivyoahidi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana katika mtaa wa Lumumba Kizza Zaidi (ambaye hakupenda kueleza kazi yake na anakoishi) alisema kuwa baraza ni zuri kutokana mabadiliko yaliyofanyika katika wizara.
"Wanawake nao safari hii wamepewa kipaumbele kama Rais Kikwete alivyoahidi kuwa wakinamama nao wana uwezo wa kufanya kazi kama wanaume," alisema Zaidi
Alisema kuwa mbali na hilo Rais Kikwete amejaribu kupunguza vitu vingine ambazo siyo vya lazima.
Naye mfanyabiashara wa Dar es Salaam Abdulrahiman Dahoma alisema baraza ni zuri kutokana na kuwa na sura mpya ambazo watajitahidi kutupa imani kwa kutuletea maendeleo.
Pia alisema kuwa baraza hilo litakuwa lawachapakazi bora kutokana na kauli ya Rais Kikwete kuwa baraza hilo litakuwa la watendaji kazi kwa kipindi cha miaka mitano kwa wale watakaozembea watabadirishwa.
"Tunaliaminia baraza hili jipya kutokana na kauli ya Rais ya kutuletea wachapakazi kwa kipindi cha muda wa miaka mitano" alisema
Nao wafanyabiashara wa vyakula ambao (majina yao hawakutaka yatajwe gazetini) walisema baraza ni zuri na wametaka walioteuliwa wasinyanyase wafanyabiashara.
Mkazi wa Dar es Salaam Khalid Salehe alitoa maoni yake kuwa baraz ni zuri lakini akaeleza kuwa Magufuli angarejeshwa kwenye Wizara ya Ujenzi ambayo sasa inaitwa Wizara ya Miundombinu.
Mfanyabiashara wa madini Hussein Mtuya alisema amelipenda baraza kutokana na mwalimu wa baraza hilo aliahidi atakuwa nalo kwa muda wa miaka mitano na atakayelegalega hatoendelea naye.
Andrew Mvela alisema katika maoni yake hawezi kuwa amelizika nalo au la mpaka baada ya mwaka mmoja atakapoona utendaji wao wa kazi.